Skip to main content

Wakwepa kodi wanalindwa, wafichua taarifa wanashtakiwa- Mtaalamu

Wakwepa kodi wanalindwa, wafichua taarifa wanashtakiwa- Mtaalamu

Wafichua taarifa ni mashujaa wa zama za sasa na wanatekeleza majukumu yao kwa maslahi ya jamii na haki za binadamu hivyo hawapaswi kushtakiwa kwa kutoa taarifa kuhusu ukwepaji kodi. #luxleaks

Hiyo ni kauli ya mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji wa utaratibu wa kimataifa wa demokrasia na haki, Alfred de Zayas aliyotoa kufuatia ripoti za kuhukumiwa kwa waliotoa taarifa kuhusu sakata la Lux.

Watu hao walifichua jinsi ukwepaji kodi unavyofanyika kwenye benki za Luxembourg ambapo de Zayas amesema yaonekana zama za sasa ni za segemnege ambapo waporaji wanalindwa huku wafichua taarifa wanashtakiwa.

Amesema iwapo ukwepaji kodi utaendelea sambamba na misamaha ya kodi, serikali hazitakuwa na uwezo wa kukidhi majukumu yao ya kusimamia haki za binadamu.

Tarehe 29 mwezi Juni mwaka 2016, wafanyakazi wawili wa zamani wa PricewaterhouseCoopers walihukumiwa kwa kosa la kuweka hadharani nyaraka zinazofichua jinsi Luxembourg inavyotoa misamaha ya kodi iliyowezesha kampuni za Apple, Ikea na Pepsi kukwepa mabilioni ya pesa za kodi.

Hata hivyo mwandishi aliyeripoti sakata hilo kwa kutumia taarifa hizo aliachiliwa huru.

Bwana de Zayas amesema mabunge yanapaswa siyo tu kupitisha sheria bora zinazolinda wafichua taarifa, bali pia kuwapa tuzo kwa kuchangia katika maadili na uaminifu.

=======