Ufadhili wa kibinadamu unapungua, misaada zaidi yahitajika kwa watu Fallujah- UM
Umoja wa Mataifa umeeleza kutiwa wasiwasi na mzozo wa kibinadamu unaoibuka huko Fallujah, nchini Iraq, ambapo watu zaidi ya 20,000 wamekuwa wakikimbia makwao tangu tarehe 22 Mei.
Katika ziara yake, Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu nchini Iraq, Lise Grande, amekutana na watu walioweza kukimbia na kufikia maeneo salama huko Ameriyat al Fallujah, mashariki mwa mkoa wa Anbar.
Bi Grande amesema walizungumza na familia za watu walioweka maisha yao hatarini na kuukimbia mji wa Fallujah, wakihadithia matukio ya kuvunja moyo.
Operesheni kubwa ya kibinadamu inaendelea, ikilenga kuwasaidia watu waliolazimika kuhama makwao Fallujah, lakini ni dola milioni 265 (asilimia 31) tu ya ombi la Umoja wa Mataifa la dola milioni 861 za kuwasaidia watu milioni 7.3 nchini Iraq ndizo zilizopatikana kufikia sasa.