Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ateua kikosi-kazi cha mizozo ya kiafya duniani

Ban ateua kikosi-kazi cha mizozo ya kiafya duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametangaza leo wanachama wa kikosi kazi chake kuhusu mizozo ya kiafya duniani.

Kikosi-kazi hicho kiliundwa na Katibu Mkuu kwa minajili ya kusaidia na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yaliyofanywa na jopo la ngazi ya juu kuhusu jitihada za kimataifa panapoibuka mizozo ya kiafya.

Jopo hilo lilitoa ripoti yake ya kwanza mnamo Februari tisa, 2016, yenye kichwa: “kulinda ubinadamu dhidi ya mizozo ya kiafya siku zijazo”, ambayo ilifuatiwa na ripoti ya Katibu Mkuu iliyotoa mapendekezo kuhusu jinsi ya kuimarisha mfumo wa afya duniani.

Miongoni mwa wanakikosi hicho ni maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa, wakiwemo Naibu Katibu Mkuu, Jan Eliasson, Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dkt. Margaret Chan, Mkuu wa UNDP, Helen Clark, na Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Anthony Lake.

Kazi ya kikosi-kazi hicho itakuwa ni kutekeleza mapendekezo ya jopo la ngazi ya juu, ikiyaoanisha na yale ya Katibu Mkuu.