Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sina uhakika bado na tarehe ya mazungumzo Syria- de Misturra

Sina uhakika bado na tarehe ya mazungumzo Syria- de Misturra

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likijikita zaidi suala la Syria ambapo limepokea taarifa ya kila mwezi ya mjumbe maalum wa Katibu Mkuu kuhusu nchi hiyo, Staffan de Misturra.

Kikao hicho kilikuwa cha faragha ambapo baada ya kumalizika de Misturra amezungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani na kueleza kuwa shambulio la kigaidi huko Istanbul, Uturuki ni kumbusho kwa wajumbe wa baraza kuwa vita dhidi ya ugaidi ni jambo linalohitaji mwendelezo.

Amesema kushinda ugaidi maeneo mbali mbali ikiwemo Syria kunahitaji mpito wa kisiasa na hiyo ndio njia pekee ya kuondoa fursa ya kushamiri kwa ugaidi.

Halikadhalika amesema ufikishaji wa misaada kwenye maeneo yaliyoshikiliwa nchini Syria umeimarika lakini bado juhudi zahitajika zaidi.

Kuhusu mchakato wa kisiasa nchini Syria hususan mazungumzo baina ya wasyria kwa lengo la kusaka suluhu la kudumu amesema..

(Sauti ya de Misturra)

"Sijapanga tarehe mahususi kwa mwezi wa Julai, na ninafanya hivyo kwa sababu nataka kuhakikisha mashauriano ninayofanya na wenyeviti wenza yanakuwa na matunda na tunapoitisha kikao kuwe na uwezekano wa kuwa na kitu Agosti. Lakini ninalenga au tunalenga ndani ya Julai lakini si kwa gharama yoyote ile na haina hakikisho. Na tunalenta mwezi Agosti tuwe na kitu mahsusi ili hatimaye Septemba tuangalie tulicho nacho.”