Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani na maendeleo mada kuu kwenye UM

Amani na maendeleo mada kuu kwenye UM

Uhusiano baina ya amani, ujenzi wa amani na maendeleo endelevu umemulikwa kwenye  mkutano wa pamoja wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Kiuchumi na Kijamii na Tume ya Ujenzi wa Amani. Priscilla Lecomte na taarifa kamili

(TAARIFA YA PRISCILLA)

Akihutubia mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson amesema kwamba, ili kudumisha amani, ni muhimu kuingiza suala hilo katika miradi ya maendeleo, kabla mizozo haijaibuka, akikumbusha kwamba mara nyingi mizizi ya mizozo ni sababu za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa Macharia Kamau, ambaye pia ni mwenyekiti wa Tume ya Ujenzi wa amani aliyeongoza mkutano huo, amesisitiza kwamba suala la ujenzi wa amani ni suala mtambuka katika ajenda ya maendeleo endelevu.

(sauti ya Balozi Kamau)

“Tukizungumza kuhusu ujenzi wa amani, tukizungumza kuhusu amani, tunazungumza kuhusu ajenda nzima ya 2030. Nimezungumza pia kuhusu umuhimu wa utawala wa sheria kwa sababu hakuna nchi ambayo inaweza kudumisha amani bila taasisi imara iliyojengwa kwa kuheshimu utawala wa sheria.”