Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgombea mwingine nafasi ya Ukatibu Mkuu UM ajieleza Baraza Kuu

Mgombea mwingine nafasi ya Ukatibu Mkuu UM ajieleza Baraza Kuu

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha kusikiliza mgombea wa 10 kati ya 11  wanaowania kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa umoja huo atakayemrithi Ban Ki-moon, ambaye anahitimisha muhula wake mwishoni mwa mwaka huu.

Mgombea huyo Miroslav Lajčák wa Slovakia ambaye katika hotuba yake tangulizi ya kurasa nne aliyotoa kabla ya kuulizwa maswali na nchi wanachama na wawakilishi wa vikundi vya kiraia amesema Umoja wa Mataifa una kila inachohitaji kutekeleza majukumu yake lakini bado kuna mizozo, ugaidi na dunia si salama kama ilivyokuwa miaka 10, 20 au 30 iliyopita.

Bwana Lajčák ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na masual ya Ulaya wa Slovakia amesema mathalani Umoja wa Mataifa una taasisi, una taratibu na kanuni, halikadhalika teknolojia na rasilimali watu lakini bado hali ni changamoto..

(Sauti ya Miroslav)

" Lakini pengine mfumo hautoshelezi kuweza kukabili changamoto za sasa kama inavyotarajiwa kutoka kwetu. Lengo langu basi litakuwa kuweka msisitizo jinsi ya kuwa na michakato yenye tija. Jinsi ya kurekebisha mfumo uwe na tija zaidi. Kwa lengo la kuwa na amani na kwa maslahi ya binadamu wote. Mabadiliko ya ndani ya mfumo yanapaswa kuendelea kuakisi mabadiliko ya mazingira ya kimataifa. Ni vyema kuhakikisha mahitaji ya dunia na uwezo wetu wa kuchukua hatua vinaenda pamoja. “ 

Bwana Miroslav pia ametaja mambo manne ambayo amesema ni muhimu wa kwa Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi ambayo ni kuzuia mizozo na kuweka usuluhishi,  maendeleo, kutetea haki za binadamu na kuwa na msimamizi mkuu wa Umoja wa Mataifa mwenye sifa za kutekeleza majukumu ya chombo hicho.