Kushirikiana na wenyeji ni suluhu bora kwa waliokimbia makwao:UN/Benki ya Dunia
Wawakilishi wa serikali kutoka Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC,Tanzania, Rwanda, Uganda na Zambia, zinazohifadhi zaidi ya watu milioni 3.4 waliokimbia kutoka eneo la maziwa makuu , wamekutana Juni 6 na 7 kubadilishana uzoefu kuhusu mikakati wanayochukua kuchagiza ushirikiano na wenyeji kama suluhu kwa watu waliokimbia makwao.
Katika ukanda wa maziwa makuu wa Afrika, idadi ya wanafurushwa makwao inaongezeka na mara kadhaa inakuwa ni hali ya muda mrefu, huku watu wengine wakisalia katika hali hiyo kwa karibu miaka 20.
Moja ya suluhu mujarabu ya tatizo la kutawanywa kwa muda mrefu ni kushirikiana na jamii za wenyeji nan chi walizoomba hifadhi.
Hayo yamejitokeza katika warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na ofisi ya mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa eneo la maziwa makuu, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na Bank ya dunia.
Wengine waliohudhuria ni pamoja na wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka serikalini na washirika muhimu wanaohusika na kusaka suluhu ya kudumu kuhusu hali ya muda mrefu ya watu kukimbia makwao kwenye ukanda wa maziwa makuu.
Serikali zimesema zinatambua kwamba kushirikiana na wenyeji kunaweza kuzaa matunda mazuri kwa wakimbizi, wakimbizi wa ndani nan chi zinazowahifadhi, lakini wakati huohuo wanatambua changamoto za kisheria, kisiasa na kifedha zinazowakabili kulifanikisha hilo.