Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano yazorotesha chanjo kwa watoto Syria

Mapigano yazorotesha chanjo kwa watoto Syria

Mapigano na ghasia vinavyozidi kushika kasi nchini Syria, fursa ya chanjo kwa watoto na kuokoa maisha ya mamilioni ya watoto inapotea, imesema taarifa ya pamoja ya Shirika la AfyaUlimwenguni(WHO) na lile la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto(UNICEF).

Taarifa hiyo ikiwanukuu wawakilishi wa ukanda huo, Dtk. Ala Alwan wa WHO Dkt. Peter Salama wa UNICEF imetolea mfano wa sitisho la muda la chanjo kutokana na ongezeko la mashambulizi wa wahudumu wa afya eneo liitwalo Idleb nchini Syria, kutokana na hofu ya usalama kwa wafanyakazi hao na raia.

Imesema mathalani Mei 31, gari la kubebea wagonjwa wa dharura katika eneo hilo linalodhaminiwa na WHO na wadau wengine wa Umoja wa Mataifa lilishambuliwa. Pia magari mawili ya wagonjwa yaliharibiwa, na hospitali ya jirani ililazimishwa kufungwa na kwa siku moja pekee zaidi ya raia 50 waliripotiwa kuuwawa wakiwamo watoto kadhaa.

Tangu mwanzo wa mwaka huu, kumeripotiwa vifo vya wafanyakzi wa afya 17 nchini Syria. Theluthi moja ya hospitali nchini Syria ndizo zinazofanya kazi imesema taarifa hiyo yaWHO na UNICEF.