Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Luteni Jenerali, Jonson Mogoa Kimani Ondieki kuwa kamanda mpya wa UNMISS

Luteni Jenerali, Jonson Mogoa Kimani Ondieki kuwa kamanda mpya wa UNMISS

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ametangaza uteuzi wa Luteni Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki wa Kenya kama kamanda mpya wa vikosi vya mpango wa Umoja wa mataifa Sudan Kusini, UNMISS.

Bwana Ondieki anachukua nafasi ya Luteni jenerali Yohannes Gebremeskel Tesfamariam wa Ethiopia ambaye atamaliza muda wake tarehe 17 Juni 2016. Katibu

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Ban akishukuru kazi nzuri iliyofanywa kwa moyo na Luteni Jenerali Tesfamariam kwenye UNMISS.

Luteni Jenerali Ondieki anajiunga na UNIMISS akiwa na ujuzi wa zaidi ya miaka 34 kwenye masuala ya kijeshi kitaifa na kimataifa , uongozi imara na uzoefu.

Alikuwa Naibu Mkuu wa majeshi ya Kenya tangu mwaka 2013, lakini kabla ya hapo alikuwa kamanda wa kitengo kwenye mpango wa Umoja wa mataifa Sudan kuanzia mwaka 2010 hadi 2011.

Bwana Ondieki ana shahada ya kwanza ya masuala ya amani na migogoro kutoka chuo kikuu cha Ahas African nchini Kenya na pia amehitimu mafunzo ya kivita kutoka chuo cha vita nchini China, na chuo cha makamanda nchini Marekani.

Luteni Jenerali Ondieki alizaliwa mwaka 1960 na ana watoto watatu.