Skip to main content

UNHCR yalaani shambulio dhidi ya kambi ya wakimbizi Syria

UNHCR yalaani shambulio dhidi ya kambi ya wakimbizi Syria

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limeeleza kushtushwa sana na ripoti za mashambulizi ya makombora dhidi ya kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Syria. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(TAARIFA YA AMINA)

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, shambulio hilo lililotokea alhamisi hii limesababisha vifo vya watu 30, wakiwemo watoto, wengine wengi wakijeruhiwa. Kambi hii iliyopo kaskazini mwa Syria inawapa hifadhi wakimbizi wa ndani 2,500.

Msemaji wa UNHCR Leo Dobbs, ameiambia Redio ya Umoja wa Mataifa kwamba shambulio hilo ni ukiukwaji dhahiri wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

(sauti ya bwana Dobbs)

Tunazisihi pande zote kuheshimu haki za msingi za binadamu za watu waliokimbia makwao ambao wanastahili kupewa ulinzi, na haikuwa hivyo katika tukio hii. Tunaunga mkono uchunguzi wowote kama ulivyotolewa wito na mkuu wa OCHA Stephen O’Brien”.

Tukio hilo limelaaniwa vikali pia na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein, akisema kwamba ni wazi kuwa kambi hiyo ililengwa makusudi.

Kwa mujibu wa UNHCR, watu wapatao milioni 6.5 ni wakimbizi wa ndani nchini Syria