Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

El Nino yaangaziwa Umoja wa Mataifa

El Nino yaangaziwa Umoja wa Mataifa

Kutoka hapa New York, Baraza la kijamii na uchumi la Umoja wa Mataifa, ECOSOC leo limekuwa na mkutano maalum kuhusu El Nino likiangazia hatari zake na jinsi ya kutumia fursa zilizopo kukabiliana na hali hiyo. Taarifa zaidi na Flora Nducha.

(Taarifa ya Flora)

Akifungua mkutano huo Rais wa ECOSOC Oh Joon amesema tangu mwaka jana, El Nino imeleta zahma kubwa huko Asia na hata Afrika, ikiwemo ukame na mafuriko ambapo Malawi ilitangaza hali ya dharura.

Amesema athari za kiuchumi na kijamii kwa nchi zilizokumbwa ziko dhahiri na hivyo hatua za pamoja ni muhimu ili kukabili na hatimaye kuweza kufanikisha ajenda 2030.

(Sauti ya Joon)

 “Wadau wote Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa, kikanda, kiraia na wanasayansi wachukue hatua za pamoja na thabiti kudhibiti athari za El nino. Tujenge uwezo wa kukabili majanga na utayari wa kuepusha madhara kwenye nchi zinazokumbwa na El Nino.”

Akihutubia mkutano huo kwa njia ya video kutoka Mexico, Robert Glasser ambaye ni mkuu wa ofisi ya Umoja wa mataifa ya upunguzaji wa hatari ya majanga UNISDR amesifu nchi ambazo tayari zinachukua hatua kusambaza taarifa za tahadhari kwa wananchi ili kupunguza athari za El Nino kwenye sekta kama vile kilimo na uvuvi.

image
Hali ilivyokuwa wakati wa mafuriko huko Benguela, kusini mwa Malawi. (Picha:Arjen van der Merwe/UNICEF)
Amesema kutokana na maendeleo ya teknolojia, kiwango au kasi ya El Nino na La Nina vinaweza kukadiriwa na hivyo sekta za kijamii na kiuchumi zikipatiwa taarifa mapema zinaweza kuokoa siyo tu uhai wa wananchi bali pia kupunguza uharibifu unaoweza kutokea.

Halikadhalika amepongeza nchi zinazochukua hatua hizo ikiwemo Ecuador na Ufilipino na pia barani Afrika ambapo nchi zinasaidia waathirika kujikimu na kupunguza makali…

(Sauti ya Glasser)

“Serikali ya Malawi inaongeza huduma za kijamii ikiwemo kuwapatia waathirika fedha kujikimu,  miradi ya umma ambayo wananchi wanafanya kazi, na kugawa mlo shuleni. Nchini Angola, wizara ya afya imeanza kuimarisha huduma za afya hasa kudhibiti homa ya manjano na Malaria na magonjwa mengine kutokana na uhusiano wao na hali ya hewa na milipuko ya magonjwa.”