Skip to main content

Kinachoendelea Syria ni ishara ya kupuuza uhai wa raia- Zeid

Kinachoendelea Syria ni ishara ya kupuuza uhai wa raia- Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, amesema kinachoendelea Syria ikiwemo mashambulizi ya hospitali na masoko kinadhihirisha jinsi pande zote kwenye mzozo huo zinavyopuuza maisha ya raia.

Ametoa kauli hiyo leo kufuatia matukio ya wiki hii ya vikosi vya serikali na vile vya upinzani kushambulia maeneo ya raia na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Zeid amesema ghasia imeongezeka katika kiwango kikubwa kuliko hata ilivyoshuhudiwa kabla ya sitisho la mapigano na kuna taarifa kuwa vikosi vya kijeshi vinajipanga kutumia silaha za sumu.

Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

(Sauti ya Rupert)

 “Kamishna mkuu pia ananyooshea kidole Baraza la Usalama kwa kushindwa mara kwa mara kupeleka suala la Syria kwenye mahakama ya kimataifa ya  uhalifu, ICC. Angalau lifanye hivyo. Katika fikra za wengi mataifa makubwa ndiyo yako nyuma ya matukio ya maelfu ya watu kupoteza maisha na  mamilioni kupoteza makazi.”