Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamati dhidi ya ubaguzi wa rangi yakagua ripoti ya Rwanda

Kamati dhidi ya ubaguzi wa rangi yakagua ripoti ya Rwanda

Kamati ya kupinga ubaguzi wa rangi imehitimisha Ijumaa hii ripoti ya pamoja ya Rwanda kuhusu utekelezaji wake wa makubaliano ya kimataifa ya kupinga aina zote za ubaguzi wa rangi.

Akiwasilisha ripoti hiyo mjini Geneva, mwakilishi wa kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa, Francois Xavier Ngarambe, amesema kwamba mauaji ya kimbari ya Watutsi mwaka 1994, ambayo yalitokana na ubaguzi, yanasalia katika kumbukumbu ya Wanyarwanda.

Ameongeza kwamba historia hiyo ni funzo kwa serikali na watu wa Rwanda ya kuweka mamlaka ambayo inahakikisha kwamba watu wote ni sawa mbele ya sheria na kwamba wana haki sawa.

Ripoti inasema kwamba serikali imechukua hatua madhubuti ya kusaida makundi ya walio hatarini katika jamii kupata huduma na kwamba hakuna kundi moja tofauti kuliko jingine.

Wataalam wamesema ni vigumu kuzungumzia ubaguzi wa rangi nchini Rwanda bila kutaja mauaji ya kimbari ya 1994 kwani mauji hayo yalijumuisha ubaguzi wa kikabila wa hali ya juu.

Halikadhalika wataalam wamepongeza hatua ambazo zimepigwa na watu wa Rwanda katika kuimarisha maridhiano na ukuaji wa kiuchumi, lakini kwa upande mwingine wametaja maamuzi ya serikali kukosa kutambua makabila kama mbinu ya kuimarisha uwiano kama sababu ya watu wa kabila la Batwa kuendelea kuteseka.

Kwa mantiki hiyo Evelyne Hohoueto Afiwa-Kindena, mtaalam huru wa Rwanda amesisitiza wito wa kamati kwamba makundi yaliyo hatarini ni lazima yalindwe na mikakati madhubuti ili kuweza kuangalia matakwa yao na kuwawezesha kufikia huduma zote za serikali.