Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na washirika wake watoa wito kusaidia watu milioni 60 walioathirika na El nino :OCHA

UM na washirika wake watoa wito kusaidia watu milioni 60 walioathirika na El nino :OCHA

Kukiwa na mamilioni ya watu duniani kote walioathirika na ukame, mafuriko na maafa mengine yatokanayo na hali ya hewa yaliyosababishwa na El Niño, jumuiya ya kimataifa ni lazima ichukue hatua sasa kushughulikia mahitaji ya kibinadamu na kuzipiga jeki katika kujijengea uwezo wa kukabiliana na zahma zitakazowafika siku zijazo.

Hayo yamesemwa na Stephen O’Brien, mratibu wa Umoja wa mataifa wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura. Amesema msimu wa sasa wa El Niño ni mbaya sana katika historian a umeathiri watu milioni 60 wakiwemo wasiojiweza barani Afrika, Amerika ya Kati na Kusini na Pacific. Bwana O’Brien amesema wakati wa kuchukua hatua ni sasa ili kuwasaidia wale ambao maisha yao yote na mustakhbali wao uko mashakani.

Hadi sasa OCHA inasema El Niño imeshaathiri uhakika wa chakula, na afya kwa familia na jamii nyingi duniani. Mpango wa usaidizi umeshakamilika kwa nchi 13 na inaomba dola bilioni 3.6 ili kukabili mahitahi ya chakula , kilimo, lishe, afya na dharura ya maji na usafi.