Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mizozo yakwamisha watoto kupatiwa chanjo - UNICEF

Mizozo yakwamisha watoto kupatiwa chanjo - UNICEF

Wakati wiki ya chanjo duniani ikianza Jumatatu ijayo, Umoja wa Mataifa umesema takribani theluthi mbili ya watoto ambao hawajapata chanjo za msingi wanaishi kwenye maeneo yenye mizozo.

Miongoni mwao ni Sudan Kusini ambayo inaongoza kwa kuwa na asilimia 61 ya watoto wasiopatiwa chanjo za msingi, ikiwa ni idadi kubwa zaidi duniani ikifuatiwa na Somalia na Syria.

Mkuu wa chanjo kwenye shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Robin Nandy amesema mizozo inaweka mazingira stahili kwa magonjwa kulipuka, mathalani miundombinu ya afya inapoharibiwa kwa makusudi au usalama unapokosekana.

Ametaja magonjwa kama surua, kuhara nay ale ya njia ya hewa kuwa sababu kubwa ya magonjwa na vifo vya utotoni, magonjwa ambayo amesema yanaweza kuzuilika kwa chanjo.

Bwana Nandy amesema kwa kukosa chanjo watoto wanaporwa afya na mustakhbali wao hivyo amesema utoaji chanjo ni huduma muhimu inayopaswa kulindwa na pande zote wakati wa mzozo.