Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa MONUSCO azungumza na walinda amani wa Tanzania kuhusu ukatili wa kingono

Mkuu wa MONUSCO azungumza na walinda amani wa Tanzania kuhusu ukatili wa kingono

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC Maman Sidikou, ametembelea hii leo kambi ya kikosi cha walinda amani wa Tanzania iliyoko Mavivi, Kivu Kaskazini.

Ziara hiyo ilifuatia tuhuma za ukatili wa kingono uliodaiwa kufanyika na baadhi ya walinda amani hao nchini humo dhidi ya wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa akaunti ya Twitter ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC MONUSCO, lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kukariri utashi wa Bwana Sidikou wa kutekeleza kanuni za Katibu Mkuu Ban Ki-moon katika kukabiliana na visa vya ubakaji na unyanyasaji wa kingono, na jinsi zisivyokubaliwa kamwe.

Bwana Sidikou ambaye pia ni mkuu wa MONUSCO, amejadiliana na walinda amani waliokuwepo kambini kwa ajili ya kusisitiza kauli hiyo, akiambatana na viongozi wa MONUSCO.

Aidha, amewatia moyo wawakilishi wa jamii wa Mavivi akiwaeleza kwamba uchunguzi unaendelea, na wahanga wanahudumiwa, na kuomba ushirikiano wa jamii katika kupambana na tatizo hilo.