Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Timu ya UM yaanza kukusanya taarifa za ubakaji CAR

Timu ya UM yaanza kukusanya taarifa za ubakaji CAR

Timu ya pamoja, ikiongozwa na Naibu Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Diane Cooper, imesafiri leo kwenda mkoa wa Kimo kwa mara ya pili, kama sehemu ya ujumbe wa kukusanya taarifa na kutafuta ukweli uliotangazwa wiki iliyopita.

Akitangaza hatua hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini New york, msemaji wa Katibu Mkuu Stephane Dujarric, amesema wajumbe hao pia wamekutana na wadau kadhaa mashinani.

Ameongeza kwamba uchunguzi wa pamoja wa ofisi ya ufuatiliaji wa ndani na nchi wanachama zinazochangia vikosi vya kulinda amani unatarajiwa kuzinduliwa katika siku chache zijazo.

“Juu ya hayo, Mratibu Maalum wa Katibu Mkuu katika kuboresha jitihada za Umoja wa Mataifa dhidi ya unyanyasaji wa kingono, Jane Holl Lute, atasafiri kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika siku chache zijazo. Hii ni ziara yake ya kwanza kunakofanyika operesheni za ulinzi wa amani tangu alipouchukuwa wadhfa huo, mnamo Machi mosi.”