Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusiwafeli watu wanaotuhitaji, wanapotuhitaji zaidi- Ban

Tusiwafeli watu wanaotuhitaji, wanapotuhitaji zaidi- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesisitiza umihimu mkubwa wa mashauriano na ushirikiano wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kufanikisha mkutano wa masuala ya kibinadamu, ambao utafanyika siku 50 tokea leo Aprili nne, jijini Istanbul, Uturuki.

Ban amesema, katika miaka mitatu iliyopita, ushiriki na michango ya nchi wanachama na wadau wengine, imesaidia kuendeleza mchakato wa mkutano huo wa kimataifa wa kiutu, ambao maandalizi yake yanaingia awamu ya mwisho, akigusia anachodhamiria kufanya,

“Kwanza, njia bora ya kufikia mabadiliko yenye ujasiri ni kuhakikisha kuwa viongozi wapo ili wayawezeshe. Ndiyo maana nitaandaa kikao cha viongozi wa nchi na wakuu wa serikali siku ya kwanza, Mei 23.”

Ban amesema kikao hicho cha viongozi kitatoa fursa ya kujadili majukumu matano muhimu ya Ajenda ya Ubinadamu.

“Majukumu hayo matano ni, mosi, uongozi wa kisiasa katika kuzuia na kumaliza mizozo; pili, kutunza kanuni zinazolinda ubinadamu; tatu, kutomwacha mtu yeyote nyuma; nne, kubadilisha maisha ya watu- kutoka kupeleka misaada hadi kumaliza uhitaji; na tano, kuwekeza kwa ubinadamu”

Ban amesema sasa kuna fursa ya kipekee ya kusimama pamoja na kutoa ujumbe kwamba hautokubalika tena mmomonyoko wa ubinadamu ambao unaonekana duniani sasa, akitoa wito

“Tusiwafeli watu wanaotuhitaji, wanapotuhitaji zaidi. Istanbul ndiyo fursa hiyo. Historia itatuhukumu kutokana na jinsi tunavyotumia fursa hii. Tusiwafeli mamilioni ya wanaume, wanawake na watoto walio katika uhitaji mkubwa. Huu ndio ujumbe ninaowatuma nao kwa nchi zenu. Njooni Istanbul katika ngazi ya juu zaidi, na kuonyesha uongozi kuhusu changamoto kubwa za karne ya 21.”