Dola milioni 105 zahitajika kuokoa maisha kwenye ukame Somalia

31 Machi 2016

Mashirika ya kibinadamu nchini Somalia yamezindua leo ombi la msaada wa dola milioni 105 kwa minajili ya kuongeza jitihada za usaidizi wa kunusuru maisha na kujenga uthabiti wa zaidi ya watu milioni moja katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame kaskazini mwa nchi. Taarifa kamili na Flora Nducha

(Taarifa ya Flora)

Ukame huo ambao makali yake yameongezwa na hali ya hewa ya El Niño, unaathiri maeneo ya majimbo ya Puntland na Somaliland, ambayo tayari yanakumbana na hali ya kibinadamu yenye rundo la changamoto.

Taarifa ya Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa (OCHA), imesema watu wapatao milioni 1.7, sawa na ailimia 40 ya idadi nzima ya watu milioni 4.6 wanaoishi katika maeneo hayo, wanahitaji usaidizi wa kibinadamu na kuinuliwa kiuchumi.

Tayari, takriban watu laki nne wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

OCHA imesema iwapo usaidizi wa fedha hautapatikana haraka, madhara ya ukame huo yatakuwa makubwa zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa msimu ujao wa mvua umetabiriwa kuwa usio na mvua tosha.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter