Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

El Nino yazidi kupanua wigo wa janga la kibinadamu Ethiopia

El Nino yazidi kupanua wigo wa janga la kibinadamu Ethiopia

Serikali ya Ethiopia kwa kushirikiana na ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini humo wanatarajia kufanya tathmini mpya ya mahitaji ya kibinadamu nchini humo kwa mwaka huu wa 2016.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa kibinadamu OCHA imesema hayo leo ikitaja msingi wa hatua hiyo ni kuzidi kupanuka kwa madhara ya kibinadamu yatokanayo na El Nino iliyosababisha ukame mkali nchini Ethiopia.

Mathalani imesema hadi sasa kuna watoto Milioni 2.2 wenye utapiamlo, wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano huku watoto 450,000 waliokumbwa na unyafuzi wakihitaji huduma maalum za lishe.

Kama hiyo haitoshi idadi ya wakulima wadogo wadogo wanaohitahi msaada wa mbegu imeongezeka kutoka Milioni 2.2 hadi Milioni 3.3.

Awali, ombi la mwezi Disemba mwaka jana la dola Bilioni 1.4 kukwamua raia Milioni 10.2 walioathiriwa na El Nino limeonyesha halitoshelezi licha ya huduma kuendelea kusambazwa.