Mfanyakazi wa UM auwawa katika shambulio Côte d’Ivoire: UNOCI
Mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa wa kujitolea Andreevska Mitrovska, mzaliwa wa iliyokuwa jamauri ya Yugoslavia ya Macedonia, ameuwawa kufuatia shambulio la jumapili Machi 13 mjini Grand-Bassam nje kidogo ya mji mkuu wa Côte d’Ivoire, Abidjan.
Kwa mujibu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Côte d’Ivoire UNOCI pamoja na mpango wa Umoja wa Mataifa wa kujitolea UNV mfanyakazi huyo alikuwa mhudumu wa kiraia katika kitengo cha uhandisi.
Shambulio lililosababisha kifo cha Bi Mitrovska lililaaniwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon. UNOCI na UNV wametuma salamu za rambirambi kwa familia yake ,marafiki na wafanyakazi wenzake.
Marehemu huyo aliwasili nchini Côte d’Ivoire mnamo Disemba 28 mwaka jana, kutekeleza wajibu wake wa Meneja wa kambi ya UNOCI iitwayo Anankouakouté. Kabla ya kuelekea nchini humo, alitumika nchini Afghanistan kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.