Bodi ya magavana wa IAEA waidhinisha Euro milioni 2.3 kusaidia vita dhidi ya Zika

Bodi ya magavana wa IAEA waidhinisha Euro milioni 2.3 kusaidia vita dhidi ya Zika

Mradi mpya wa Euro milioni 2.3 utazisaidia nchi za Amerika ya Kusini na Caribbean kupambana na virusi vya Zika kwa kutumia utaalamu wa nyuklia ambao umeshatumika kukabiliana na wadudu mbalimbali, kwa mujibu wa uamuzi wa bodi ya magavana wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki IAEA.

IAEA itatoa msaada wa vifaa na mafunzo kwa wafanyakazi wa maeneo hayo ya jinsi ya kutumia mbinu hiyo dhidi ya mbu wa Aedes ambao wanabeba virusi vya Zika. Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa IAEA Yukiya Amano, mradi huo mpya unaimarisha mikakati ya kitaifa na kikanda ya kudhibiti ongezeko la mbu aina ya Aedes .

Shirika hilo litapeleka mbinu hiyo ambayo inawanyanya wadudu kuwa tasa (SIT) ambayo ni dawa ya kudhibiti wadudu inayotumia mionzi. Mionzi hiyo itatumiwa katika kituo maalumu na itawafanya mbu dume wa Aedes kuwa tasa hali ambayo itadhibiti kuzaliana kwa mbu hao.

IAEA pia inasaka fedha kutoka kwa nchi wanachama ili kufadhili mradi huo mpya kwa miaka minne kuanzia mwezi Aprili mwaka huu. Mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la afya duniani WHO, PAHO na sekta za afya za kitaifa.