Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuangazie mizozo kwa macho ya kisasa, siyo vita baridi tena: mkuu wa OSCE

Tuangazie mizozo kwa macho ya kisasa, siyo vita baridi tena: mkuu wa OSCE

Hatushuhudii kurejeshwa kwa vita baridi, mizozo ya leo ni ya aina mpya na tunapaswa kuiangazie na macho ya kisasa, amesema leo Waziri wa mambo ya nje ya Ugerumani, Frank-Walter Steinmeier ambaye pia kwa mwaka huu ni Mwenyekiti wa Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya OSCE.

Amesema hayo akihutubia kikao cha Baraza la Usalama kuhusu ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na OSCE, akisema kwamba ushirikiano huo unapaswa kuimarishwa ili kukabiliana na mizozo inayoikumba dunia siku hizi, akiongeza kwamba mashirika hayo mawili yameundwa kwa ajili ya kutatua mizozo na kukuza mazungumzo baina ya nchi.

Aidha ameongeza kwamba atazingatia umuhimu wa haki za binadamu wakati wa uwenyekiti wake, pia umuhimu wa kupambana na ubaguzi na unyanyasaji akisema

(Sauti ya Waziri Steinmeier)

“ Naamini kwamba tunahitaji kuongeza bidii zaidi ili kupambana na ubaguzi wa rangi, unyanyasaji na ukosefu wa stahamala kote Ulaya, ikiwemo kwenye nchi yangu! Huko Ugerumani, ukarimu wa raia katika kuwapokea na kuwasaidia wakimbizi umesahaulika kwa sababu ya mashambulizi ya kibaguzi. Ni Vitendo vinavyochukiza ambavyo hatupaswi kuvikubali.”