Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama kujadili mwelekeo mpya wa ulinzi wa amani:Churkiy

Balozi Vitaly Churkin. (Picha:UN/Evan Schneider)

Baraza la usalama kujadili mwelekeo mpya wa ulinzi wa amani:Churkiy

Rais wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Juni Balozi Vitaly Churkin wa Urusi amesema mjadala wa wazi kuhusu mwelekeo wa shughuli za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa utakuwa ni moja ya kazi zitakazomulikwa kwa kipindi hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York wakati wa kuwaeleza mpango wa kazi, Balozi Churkin amesema mjadala huo utafanyika tarehe 11 mwezi huu na Katibu Mkuu Ban Ki-Moon atahutubia.

“Tunatarajia mjadala wetu kujikita zaidi kwenye mambo kama vile teknolojia mpya za silaha kwene ulinzi wa amani na ushirikiano baina ya ujumbe mbali mbali. Tunafikiri kuwa mjadala huu utakuwa wa manufaa kwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa."

Halikadhalika amesema licha ya kwamba ni kando ya ratiba rasmi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakuwa na kikao chake cha kila mwaka na Baraza la amani na usalama la Muungano wa Afrika, AU na kikao hicho kitafanyika New York.

Amesema pande mbili hizo zitajadili masuala ya ushirikiano hasa kwenye amani na usalama barani Afrika.