Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwekeza katika kuzuia migogoro kuna gharama ndogo kuliko kuitatua- Balozi Kamau

Kuwekeza katika kuzuia migogoro kuna gharama ndogo kuliko kuitatua- Balozi Kamau

Mwakilishi wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa Macharia Kamau, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Ujenzi wa Amani, amesema leo kuwa kuwekeza katika kuzuia mlipuko wa mzozo kuna gharama ndogo na ni endelevu zaidi kuliko jitihada za kukabiliana na mizozo tu.

Balozi Kamau amesema hayo wakati wa mjadala wa wazi katika Baraza la Usalama, ambao umehusu kufanyia tathmini mfumo wa ujenzi wa amani, ambapo ameeleza umuhimu wa kamisheni hiyo anayosimamia

“Kamisheni ya ujenzi wa amani inaweza kuchangia katika kuzuia kuanza, kuenea, kuendelea na kurejelewa kwa mzozo, kama ilivyosadikiwa katika azimio namba 2171 la Baraza la Usalama kuhusu kuzuia mizozo, lililopitishwa mnamo 2014.”

Aidha, Balozi Kamau amesema kujenga amani ya kudumu kunahitaji ufadhili wa kutosha, endelevu na wa kuhakikishiwa ili kushughulikia mizizi ya migogoro.

Mchango wa mfuko wa ujenzi wa amani katika kutoa ufadhili kwa nchi zinapoomba usaidizi umedhihirika wazi, lakini bado haujaonyesha matokeo yapasayo. Ni dhahiri kuwa mfuko huo unahitaji kuimarishwa. Tungependa kutoa wito kwa nchi zote wanachama, kufikikiria kuhusu kuongeza ahadi zao za utoaji fedha kila mwaka kwa mfuko wa pamoja katika kusaidia amani endelevu”