Skip to main content

Kikosi kazi kuhusu usaidizi wa kibinadamu Syria chakutana Geneva

Kikosi kazi kuhusu usaidizi wa kibinadamu Syria chakutana Geneva

Huko Geneva, Uswisi, kikosi kazi kuhusu jinsi ya kufikisha misaada ya kibinadamu huko Syria, kinakutana kwa mara ya pili kutathmini hali ya sasa ya ufikishaji misaada hiyo hasa kwenye maeneo yaliyozingirwa.

Kikao cha leo kinafanyika baada ya msafara wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na shirika la msalaba mwekundu la Syria kuweza kufikisha misaada muhimu kama vile vyakula, chanjo na maji kwenye miji mitatno iliyokuwa na wahitaji zaidi wiki iliyopita.

Staffan de Mistura, ambaye ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria na pia mwenyekiti wa kikao hicho amesema umoja wa mataifa unapimwa uwezo wake kutoa misaada sambamba na pande kinzani kwenye mzozo huo kuwezesha misaada kufika.

De Mistura amesema zaidi ya watu 400,000 wanaishi maeneo yanayozingirwa na vikosi vya serikali na upinzani na wanakabiliwa na shida kubwa.

Ufikishaji wa misaada wiki iliyopita uliwezekana kufuatia majadiliano yaliyoongozwa na kikundi cha kimataifa cha usaidizi wa Syria, ISSG kilichokutana Munich Ujerumani.