Skip to main content

UNICEF yatoa kauli mashambulizi dhidi ya hospitali ya watoto Syria

UNICEF yatoa kauli mashambulizi dhidi ya hospitali ya watoto Syria

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeeleza kushtushwa kwake na ripoti za mashambulizi dhidi ya vituo vinne vya afya nchini Syria, ambapo viwili kati ya hivyo vinapatiwa msaada na shirika hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Anthony Lake amesema katika taarifa yake kuwa moja ya vituo hivyo ni ya watoto na wazazi ambako watoto kadhaa wameripotiwa kuuawa na wengine wamelazimika kuhamishwa.

Mashambulizi mawili ya anga yalifanyika huko Azaz mjini Aleppo na mengine mawili huko Idlib ambako hospitali moja imeripotiwa kupigwa makombora mara mbili.

Ripoti zaidi zinasema shule mbili zilishambuliwa huko Azaz na watoto sita wameripotiwa kuuawa ambapo UNICEF imesema inasaka taarifa zaidi.

UNICEF inasema theluthi moja ya hospitali nchini Syria sambamba na robo  ya shule hazifanyi kazi.

Kwa mantiki hiyo UNICEF imesema kando ya kushinikiza diplomasia na wahusika kuwajibika kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu, inakumbusha wahusika kuwa wahanga wa janga linaloendelea ni watoto.