Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msafara wa chakula wa WFP wawasili Taiz Yemen

Msafara wa chakula wa WFP wawasili Taiz Yemen

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa WFP limefanikiwa kuwasilisha chakula kwa watu 18,000 ndani ya eneo lililoghubikwa na mapigano la Taiz nchini Yemen ambako wakaazi wanahitaji haraka msaada wa chakula.

Hii ni mara ya pili WFP inapata fursa ya kuingia eneo la vita la Al Qahira kwa mwaka huu. Shirika hilo limekuwa likipeleka msaada wa chakula katika baadhi ya sehemu za Taiz tangu Disemba mwaka jana likiwafikia maelfu ya watu wanaohitaji haraka msaada wa chakula, lakini kutokana na mapigano yanayoendelea imekuwa vigumu kusafirisha chakula kufikia wilaya zote.

Taiz ni moja ya majimbo 10 kati ya majimbo yote 22 ya Yemen ambayo yako katika hali mbaya ya chakula karibu kufikia baa la njaa. Kwa mujibu wa tathimini ya mahitaji ya kibinadamu ya Umoja wa mataifa kwa mwaka 2016, watu milioni 7.6 nchini Yemen wanakabiliwa na uhaba wa chakula na wanahitaji msaada wa haraka.