Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Aleppo na maeneo mengine Syria inatisha- Zeid

Hali Aleppo na maeneo mengine Syria inatisha- Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Bindamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, ameelezea kusikitishwa mno na hali ya haki za binadamu inayozorota kasi ndani na nje ya mji wa Aleppo na maeneo mengine nchini Syria, ambako amesema ukiukwaji wa haki unaoshtua unafanyika kila siku. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Akikumbusha pande zote kuhusu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa, wa kuwalinda raia wakati wote na kuwezesha ufikishaji wa misaada, Kamishna Zeid amesema kulazimu utapia mlo kwa raia kama mbinu ya vita ni ukiukwaji dhahiri wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu. Cecile Poully ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Geneva.

(Cecil Poully)

“Tunalaani vitendo hivi ukiukwaji huu vikali. Ni bayana kuwa pande zinazozozana nchini Syria hazijali hata kidogo mauaji na uharibifu zinazofanya nchini humo.”

Amesema tangu mashambulizi yalipoanza kufanywa na serikali wiki iliyopita, yakiwemo mashambulizi ya angani yanayofanywa na ndege za Urusi na Syria, raia 15,000 wamefurushwa makwao, na wengine 300,000 wanakabiliwa na hatari ya kuzingirwa.