Mivutano ya kikabila yaongezeka DRC: UM

Mivutano ya kikabila yaongezeka DRC: UM

Ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza kushtushwa sana na ripoti za kuongezeka kwa mivutano ya kikabila kwenye maeneo ya ya Lubero na Walikale huko jimbo la Kivu Kaskazini, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC.

Taarifa ya ofisi hii imeeleza kwamba watu angalau 21 wameuawa, 40 wamejeruhiwa na nyumba 70 kuteketezwa kwa kipindi cha mwisho wa juma.

Aidha watu wengi wameripotiwa kulazimika kuhama makwao, huku uporaji ukiripotiwa halikadhalika visa vitatu vya ubakaji , Ofisi ya Haki za Binadamu ikionya kwamba mivutano hiyo baina ya watu wa jamii za wahutu na wanande iliyokuwa ikiongeza tangu Novemba 2015 sasa imefika kiwango cha kushutusha hadi kuweza kusababisha kiwango kikubwa cha ghasia.

Ofisi ya Haki ya za Binadamu imeeleza kwamba watu wa jamii hizo wanasaidiwa na vikundi vya waasi wa FDLR na Mayi Mayi, ikiiomba serikali ya DRC kujitahidi kulinda raia na kuondoa vitisho vya vikundi vilivyojihami.