Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano yaibua mahitaji mapya ya kibinadamu Equatoria Magharibi, Sudan Kusini

Mapigano yaibua mahitaji mapya ya kibinadamu Equatoria Magharibi, Sudan Kusini

Watu wapatao 50,000 wanahitaji usaidizi wa kibinadamu huko Mundri, katika jimbo la Equatoria Magharibi, nchini Sudan Kusini, kufuatia mapigano katika miezi michache iliyopita.

Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA, ambalo limeongeza kuwa jitihada za kibinadamu zimetatizwa na kuendelea kuwepo hali tete kiusalama, huku wadau wa kibinadamu wakiendelea kusaka kuhakikishiwa kuwa wanaweza kufikisha misaada salama.

Wadau wa kibinadamu waliweza kufikisha misaada mnamo mwezi Disemba 2015 kwa watu 10,000 walioathiriwa katika eneo hilo. OCHA imesema kuwa hivi sasa wanagawa bidhaa muhimu za nyumbani na vifaa vya makazi kwa watu wapatao 17,500 waliomo hatarini zaidi kwenye kaunti ya Mundri Magharibi, wakiwemo waliopoteza mali zao ama kwa uporaji au kuteketezwa moto.