Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madai zaidi ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto CAR yajitokeza:Zeid

Madai zaidi ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto CAR yajitokeza:Zeid

Kamishina Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa mataifa  Zeid Ra’ad Al Hussein Ijumaa amesema  ana wasiwasi mkubwa kwa sababu ya kuendelea kwa madai ya unyanyasaji wa kingono nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) unoafanywa na vikosi vya kigeni.

Tuhuma hizo zinasemekana kufanyika mwaka 2014, lakini zimebainika tu katika wiki za karibuni. Timu ya pamoja ya Umoja wa Mataifa CAR hivi karibuni imewahoji wasichana kadhaa waliosema wamenyonywa au kunyanyaswa kingono na askari wa vikosi vya kigeni.

Wasichana hao waliokuwa na umri wa miaka kati ya 14 na 16 wakati wa matukio,  wawili kati ya hao wanne walisema walibakwa na wengine wawili walidai kulipwa pesa ili kuwa na uhusiano wa kingono na wanajeshi ambao ni sehemu ya kikosi cha muungano wa Ulaya EUFOR Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu

(Sauti ya Rupert)

"Msichana na mvulana walio na umri wa miaka saba na miaka tisa mtawalia, walitendewa unyanyasaji unaodaiwa kutekelezwa 2014. Msichana alisema alifanyishwa vitendo vya kingono na askari kutoka Ufaransa na kupewa chupa ya maji na pakiti ya biskuti. Wawili hao walisema kwamba walinyanyaswa pamoja na watoto wengine kwa njia kama hiyo. Kamishna mkuu anasema kwamba, uhalifu kama huo hutendeka bila hatua zozote kuchukuliwa, huku wanaotekeleza vitendo hivyo wakiwa hawawajibishwi. Mataifa yana wajibu wa kuchunguza, kushtaki na kuhakikisha kwamba wahanga wanafidiwa."

Wakati kesi zilizotajwa na kamishina mkuu zinahusiana na vikosi ambavyo sio vya Umoja wa mataifa, idadi ya visa vingine vinavyohusisha walinda Amani wa Umoja wa mataifa vimejitokeza wakati wa mahojiano yaliyofanywa na timu ya pamoja na Umoja wa mataifa.