Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msimu wa baridi wakumba watoto wanaokimbilia Ulaya

Msimu wa baridi wakumba watoto wanaokimbilia Ulaya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF limeonya kwamba watoto wanaokimbia barani Ulaya wanakumbwa na madhara ya msimu wa baridi, ikiwemo vichomi vikali yaani pneumonia na ugonjwa wa kuhara.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo UNICEF imeeleza kwamba watoto hawa hawana nguo za kuwakinga na baridi kali na theluji, na sehemu wanakolala hazina joto la kutosha.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac amesema kwamba licha ya kukumbwa na changamoto kutokana na kasi ya uhamiaji wa familia hizo, UNICEF imeweza kufikia watoto wapatao 100,000 Kusini Mashariki mwa Ulaya.

(sauti ya Bwana Boulierac)

“ Hadi leo UNICEF na wadau wake wameweza kufikia watoto 100,000 kwenye iliyokuwa Jamhuri ya Yugoslavia, Macedonia, Serbia, na Croatia, wakiwemo 81,000 wamepata huduma kupitia vituo rafiki kwa watoto vilivyoandaliwa kwa msimu wa baridi, na karibu watoto wachanga 18,000 wamepata huduma maalum miongoni mwa watoto wadogo.”

UNICEF imeongeza kuwa idadi ya watoto miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji imezidi kuongezeka, ifika zaidi ya theluthi moja.