Skip to main content

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa laadhimisha miaka 70

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa laadhimisha miaka 70

Leo ikiwa ni miaka 70 tangu kufanyika kwa mara ya kwanza kwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema Baraza hilo limekuwa jukwaa la watu wote. Taarifa zaidi na Grace Kaneyia.

(Taarifa ya Grace)

Nats…

Huu ulikuwa ni ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini London, Uingereza, tarehe 11 Januari mwaka 1946, ambapo nchi 51 wanachama awa kwanza wa chombo hicho walichagua Rais wao.

Na hii leo akihutubia maadhimisho maalum yaliyofanyika mjini New York Marekani Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema Baraza linazidi kuwa muhimu kwa maendeleo na amani ya kimataifa

(Sauti ya Bwana Ban)

“Maazimio yanayopitishwa na Baraza Kuu huenda hayatekelezwi mara moja lakini yanaonyesha msimamo wetu wa pamoja kuhusu changamoto kubwa za zama hizi. Maazimio hayo yanasimulia msimamo wetu. Yanaonyesha Imani yetu kwamba nchi zote duniani zikishirikiana zinaweza kutimiza zaidi kuliko zingefanya pekee yao.”

Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu Mogens Lykketoft ambaye wiki hii naye ametimiza umri wa miaka 70, amesema mkutano huo wa kwanza wa Baraza Kuu umekuwa hatua muhimu katika kujenga jamii ya kimataifa.

Ameongeza kwamba nchi za dunia zimechagua kutumia baraza hilo kujenga amani ya kimataifa:

(Sauti ya Bwana Lykketoft)

“ Kupitia Baraza Kuu, wamejenga eneo la pekee ambapo sauti za watu wote duniani zinaweza kusikika. Hata hivyo wakati wa mkutano wa kwanza, maeneo mengi ya dunia, hasa Afrika, yalikuwa yanatawaliwa na ukoloni, Leo, nchi wanachama 193 zinawakilisha asilimia 99.5 ya idadi ya watu duniani na Baraza Kuu limekuwa baraza linalowakilisha zaidi dunia siku hizi.”