Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CAR: kikosi cha walinda amani cha DRC charudishwa kwao

CAR: kikosi cha walinda amani cha DRC charudishwa kwao

Kikosi cha walinda amani kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC kilichokuwa kimetumwa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwenye Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSCA kitarudishwa DRC.

Hii ni kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ambaye amezungumza leo na waandishi wa habari mjini New York Marekani, akieleza kwamba maamuzi hayo yamefuatia tathmini zilizofanyika na idara ya Umoja wa Mataifa ya operesheni za kulinda amani mwezi Novemba kabla kikosi hakijaanza majukumu yake mwezi Disemba.

Bwana Dujarric amesema tathmini zimeonyesha kwamba kikosi hicho kilikuwa hakitimizi viwango vya Umoja wa Mataifa kwa upande wa vifaa, utayari na uchunguzi , na hivyo kitarudishwa DRC bila kuwekwa kikosi mbadala

Hata hivyo amesema Umoja wa Mataifa unatambua mchango wa vikosi vya DRC katika ulinzi wa amani nchini DRC, kupitia Ujumbe wa Muungano wa Afrika na ule wa Umoja wa Mataifa, akisema mchango huo umesaidia raia wa CAR katika wakati huu mgumu kwa nchi hiyo.