Skip to main content

Ban Ki-moon apongeza Rais Museveni na Muungano wa Afrika kwa mazungumzo ya amani Burundi

Ban Ki-moon apongeza Rais Museveni na Muungano wa Afrika kwa mazungumzo ya amani Burundi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha kuanzishwa upya kwa mazungumzo ya kisiasa baina ya pande kinzani za Burundi nchini Uganda.

Kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu amepongeza jitihada za Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye ni mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mazungumwo hayo.

Bwana Ban amezisihi pande za mzozo wa Burundi kushiriki kikamilifu kwenye mazungumzo hayo ili kukabili changamoto za kisiasa zinazoikumba nchi hiyo. Aidha amewaomba viongozi wa Burundi kuwajibika na kuipa kipaumbele amani na maridhiano.

Halikadhalika Bwana Ban amepongeza Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika kwa jitihada zake katika kusaidia serikali na raia wa Burundi kutatua mzozo huo, ikiwemo kupitia kutuma Ujumbe wa Muungano huo, MAPROBU, nchini humo.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa suluhu kwa mzozo wa Burundi ni mazungumzo jumuishi yanayoheshimu makubaliano ya Arusha na Katiba ya Burundi.

Mazungumzo yaliyofanyika mjini Entebbe nchini Uganda tarehe 28 Disemba yalihudhuriwa na Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Burundi Jamal Benomar.