Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL au Da’esh yajumuishwa na Al Qaeda kwenye vikwazo

ISIL au Da’esh yajumuishwa na Al Qaeda kwenye vikwazo

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja leo limepitisha azimio linalojumuisha kikundi cha kigaidi cha ISIL au Da’esh kwenye kamati ya vikwazo ya Al Qaeda.

Kwa mantiki hiyo kuanzia sasa itaitwa Kamati ya orodha ya vikwazo dhidi ya ISIL au Da’esh na Al Qaeda ikijumuisha vikwazo kama vile kukamata mali, zuio la safari na vikwazo vya silaha kwa vikundi hivyo na watu wote wanaohusiana nao.

Azimio limetaja vigezo vya kubaini washirika wa ISIL na Al Qaeda kuwa ni pamoja na kushiriki kwenye mipango yao kama vile kuajiri, kuwapatia fedha au silaha.

Mathalani katika zuio la safari,  nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimeombwa kuzingatia orodha ya vikwazo dhidi ya ISIL na Al qaeda pindi zinapotathmini maombi ya vibali vya kuingia kwa nchi zao.

Mapema akizungumza kabla ya kupitishwa kwa azimio hilo, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameunga mkono azimio hilo huku akipendekeza mambo matano ikiwemo ushirikiano wa kimatafa katika kubadilishana taarifa na utaalamu wa kuzuia biashara ya mali za turathi, pili kupanua wigo wa mipango ya umoja huo ya kudhibiti upatiaji fedha magaidi na tatu..

Ni lazima tushirikiane kwa karibu na sekta binafsi na ile ya kujitolea kubaini miamala inayoleta shuku na kuwekeza katika mifumo dhibiti ili kuzuia fedha zinazokwenda kwa magaidi.Nne nimeazimia kama nilivyoombwa na Baraza kuongoza mijadala ndani ya Umoja wa Mataifa kuhusu vitisho vitokanavyo na upatiaji fedha magaidi na kuwapatia taarifa ndani ya siku 45.”

Katika pendekezo lake la Tano, Ban amesihi jamii ya kimataifa kuhakiksha kampeni dhidi ya magaidi haileti machungu kwa wahamiaji, wakimbizi na jamii wanazotoka.

Kikao hicho cha Baraza la Usalama kilihudhuriwa na mawaziri wa fedha wa nchi zenye ujumbe katika baraza hilo.