WHO yaendelea kupambana na kipindupindu Iraq

WHO yaendelea kupambana na kipindupindu Iraq

Shirika la Afya duniani WHO limesema idadi ya visa vya kipindupindu nchini Iraq inaanza kupungua huku shirika hilo likiendelea kupambana na mlipuko huo.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, WHO imesema visa 4,858 vimeripotiwa na watu wawili wamefariki kutokana na mlipuko huo tangu tarehe 15 Septemba, mwaka huu na  kipindupindu kinachoiathiri Iraq ni aina ya Vibrio cholera 01 Inaba ambayo inatibiwa na antibiotiki za kawaida.

Hata hivyo sampuli zingine zimetumwa kwenye maabara ya Pasteur nchini Ufaransa kwa utafiti zaidi.

Halikadhalika WHO imesema  wilaya 16 miongoni mwa wilaya 19 za mji mkuu Baghdad zimeathiriwa na mlipuko wa kipindupindu lakini asilimia 89 ya visa vyote vimeripotiwa kwenye wilaya 10 tu zinazopakana na mto Euphrates.