Mashambulizi dhidi ya raia ni uhalifu wa kivita: MINUSCA

17 Novemba 2015

Mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati,CAR Aurélien A. Agbénonci  pamoja na jumuiya ya misaada ya kibinadamu nchini humo, wamelaani vikali mfulululizo wa mashambulizi dhidi ya wakimbizi wa ndani katika kambi za Batangafo na Bambari.

Taarifa ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini CAR, MINUSCA inasema mashambulizi hayo ya ghafla mnamo Novemba  10 na 11 yamesababisha vifo vya watu 10 na kujeruhi kadhaa huku makazi zaidi ya 700 kuchomwa moto katika kambi ya Batangafo inayohifadhi zaidi ya wakimbizi 30,000.

Taarifa inasema kuwa maelfu wamekimbia makazi hayo ya muda wakati ambapo kambini Bambari watu watatu wamekufa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa.

Bwana Agbénonci amezikumbusha pande kinzani kuwa mashambulizi dhidi ya raia ni uhalifu wa kivita na kuzitaka kuheshimu haki ya kuishi.