Pamoja tutaleta amani Libya: Kobler

Pamoja tutaleta amani Libya: Kobler

Mkuu mpya wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL aliye pia mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UM nchini humo Martin Kobler ameanza kazi yake leo kwa kuelezea matumaini aliyonayo kuhusu amani  ya taifa hilo.

Katika taarifa yake, Kobler ambaye awali alikuwa mkuu wa ujumbe wa UM nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC,  amesema ana matumaini ya kufanya kazi pamoja na walibya ambao wanahitaji  amani na kuongeza kuwa ni kupitia majadiliano na umoja ndiyo vyaweza kufikia uendelevu na kurejesha mamlaka ya kitaifa.

Amesema anafurahia ujasiri wa watu wa Libya kwani wamevumilia mengi kutokana na machafuko, hali mbaya ya kibinadamu na tishio la ugaidi vinavyoendelea.

Kobler amesema Umoja wa Mataifa na walibya wanawajibika kuimarisha hali ya kiuchumi na kibinadamu na kushughulikia haki za binadamu.