Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuhuma mpya za ukatili wa kingono zakabili walinda amani huko CAR

Tuhuma mpya za ukatili wa kingono zakabili walinda amani huko CAR

Ripoti zimetolewa hii leo kuhusu vitendo vya ukatili wa kingono , unyanyasaji na mahusiano ya kindugu vinavyodaiwa kufanywa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa dhidi ya raia huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini CAR, MINUSCA umesema kesho Alhamisi unatuma timu yake kwenda eneo husika ili kupata taarifa zaidi, kuzungumza na askari husika na kuchukua hatua  haraka ikiwemo zile za kinidhamu.

Mwakilishi wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo ambaye pia ni mkuu wa MINUSCA Parfait Onanga-Anyaga baada ya kusikia tuhuma hizo amelaani vikali akisema vitendo vya aina hivyo havikubaliki kwenye ujumbe wa taasisi hiyo.

Amesema atahakikisha haki inatendeka na kwamba azma yake ya kushughulikia suala hilo haina mchezo.

Bwana Onanga-Anyanga licha ya kutambua kuwa walinda amani hao wanafanya kazi katika mazingira magumu na vifaa vichache, amesema hali hiyo siyo kisingizio cha kufanya vitendo hivyo vya kuchukiza.

Hata hivyo ameeleza masikitiko yake kuwa tuhuma za ukatili wa kingono dhidi ya raia zinaendelea kuibuka licha ya sera ya uwazi ya MINUSCA isiyovumilia kabisa vitendo hivyo sambamba na harakati za kuzuia, kuchunguza na kuwajibisha wahusika.