Skip to main content

Vifo vya wajawazito vimepungua kwa asilimia 44 tangu mwaka 1990:Ripoti

Vifo vya wajawazito vimepungua kwa asilimia 44 tangu mwaka 1990:Ripoti

Ripoti mpya iliyotolewa leo kwa pamoja na mashirika mbali mbali ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kwamba idadi ya vifo vya wajawazito imepungua kwa asilimia 44 tangu mwaka 1990 hadi mwaka huu. Takwimu hizo zinamaanisha ni kutoka zaidi ya vifo 500,000 hadi 300,000.Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, Daktari Lale Say, Mratibu wa masuala ya afya ya uzazi kwenye Shirika la Afya Duniani WHO amesema ukanda wa Asia Mashariki umepata mafanikio makubwa zaidi, huku changamoto kubwa bado ikiwa ni Afrika ambako hutokea theluthi mbili za vifo vyote vya wajawazito.

Amesema suluhisho ni upatikanaji wa huduma bora za afya ili kuokoa maisha ya wanawake hao, ikiwemo huduma za kujisafi, kufuatilia kiwango cha shinikizo la damu na kudhibiti hatari ya kupoteza damu nyingi baada ya kujifungua.

(Sauti ya Dkt Say)

“ Tunapaswa kushirikiana na wadau wetu ili kuondoa vikwazo vinavyozuia wanawake kupata huduma bora za afya ya uzazi, vikiwa ni umaskini, umbali wa kupata huduma, ukosefu wa uelewa, mifumo duni ya huduma za afya au mila potofu.”

Vifo vya wajawazito ni vifo vinavyotokea wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na hadi wiki sita baada ya kujifungua.