Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sierra Leone yajiandaa kutangaza mwisho wa mlipuko wa Ebola

Sierra Leone yajiandaa kutangaza mwisho wa mlipuko wa Ebola

Taifa la Sierra Leone linajiandaa kutangaza mwisho wa mlipuko wa Ebola, limesema Shirika la Afya Duniani, WHO. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Tangazo la mwisho wa maambukizi ya Ebola linatarajiwa mnamo Jumamosi, iwapo hakutakuwa na visa zaidi vya maambukizi ya kirusi cha Ebola kuanzia sasa hadi Jumamosi, na hivyo kuhitimisha wiki saba za kutokuwepo visa vya Ebola nchini Sierra Leone.

Katika mahojiano na Redio ya Umoja wa Mataifa, afisa wa WHO, Fadelah Chaib, ameeleza ni kigezo gani kinatumiwa kutangaza mwisho wa maambukizi ya Ebola.

Sauti ya Fadelah Chaib

Kigezo ni kwamba kusiwe na kisa kinachorekodiwa kwa zaidi ya siku 42, na hivi ndivyo ilivyo Sierra Leone. Kwa wiki saba, hakujarekodiwa kisa kipya nchini humo, na hizi ni habari nzuri sana, kwa hiyo tunatumai kuwa leo Novemba 6 hakuna kitakachofanyika, na kisha kesho kutakuwa na hafla rasmi kusherehekea habari hizi nzuri.”

Licha ya habari hizo nzuri, WHO imesisitiza kuwa kuendeleza uangalifu kunahitajika ili kukomesha kulipuka tena homa hiyo, kwani kirusi cha homa ya Ebola, ambacho kufikia sasa kimewaua watu 11,300, kinaweza kuzuka tena.