Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yapambana na kipindupindu Iraq

UNICEF yapambana na kipindupindu Iraq

Nchini Iraq, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF linashirikiana na serikali na wadau wengine ili kupambana na mlipuko wa kipindupindu likiwa na hofu ya kuona idadi ya visa nchini humo ikiongezeka.

Tayari watu zaidi ya 2,000 wameambukizwa kipindupindu kwenye majimbo 15 miongoni mwa 18 yaliyopo nchini humo, na hadi sasa serikali imekataza wanafunzi kurudi shuleni kwenye baadhi ya maeneo ya nchi.

Kwenye taarifa yake iliyotolewa leo, UNICEF imeeleza kuwa huenda mlipuko ukaendelea kuongezeka kwa sababu ya ukosefu wa usalama na mvua kubwa.

Akizungumza na redio ya Umoja wa Mataifa, Karim Elkorany, msemaji wa UNICEF nchini Iraq, amesema licha ya changamoto nyingi katika kufikia watu walioathirika na mzozo, UNICEF imefanikiwa kufikisha misaada.

(Sauti ya bwana Elkorany)

“ Tunasaidia kusambaza maji ya kunywa kupitia chupa na malori. Tumeandaa tanki za maji za jamii na tunasambaza maji kwa familia. Tunafanya kazi na jamii ili kuwaelimisha kuhusu jinsi ya kujikinga na kutibu ugonjwa huu ili kusitisha mlipuko huo. Pia tunasambaza vidonge vingi vya chumvi ya kuongeza maji mwilini kwa ajili ya wagonjwa waliougua tayari na kuathirika na ukosefu wa maji mwilini.”