Skip to main content

Wataalam wa UM waonya kuhusu sheria ya Brazil dhidi ya ugaidi

Wataalam wa UM waonya kuhusu sheria ya Brazil dhidi ya ugaidi

Wataalam wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, wameonya kuwa mswada wa sheria dhidi ya ugaidi unaojadiliwa sasa na bunge la Brazil huenda ukazuia ufurahiaji wa uhuru wa msingi, kwani sheria hiyo inajumuisha mambo mengi sana.

Wataalam hao wamesema kuwa ufafanuzi wa uhalifu kulingana na mswada huo wa sheria huenda ukasababisha mkanganyo kuhusu ni nini serikali inatafsiri kama uhalifu wa kigaidi, na hivyo kukiuka haki za binadamu na uhuru wa msingi.

Sheria hiyo inalenga kufafanua uhalifu wa ugaidi nchini Brazili, na pia kuweka vigezo vya kuchunguza na kuwashtaki washukiwa. Sheria hiyo ilipitishwa mnamo Oktoba 28 2015 na bunge la Seneti la Brazil kwa kura 34 dhidi ya 18, na sasa inakwenda kwenye bunge la chini kujadiliwa.

Wataalam hao wameeleza masikitiko yao kuwa mswada wa sasa haujajumuisha vipengele vinavyoweka mfumo muhimu wa kulinda uhuru wa kushiriki maandamano ya kisiasa na mavuguvugu ya kijamii kuwekwa chini ya sheria hiyo.