Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watekwa nyara 13 waachiliwa huru Sudan Kusini

Watekwa nyara 13 waachiliwa huru Sudan Kusini

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umekaribisha kuachiliwa huru kwa wafanyakazi 13 waliokuwa wametekwa nyara na waasi tangu tarehe 26, Oktoba.

Wafanyakazi hawa walikuwa wakiendesha boti za UNMISS zilizokuwa zikisafirisha mafuta wakati ambapo zilivamiwa na waasi wa SPLA – upinzani. Walinda amani 18 walitekwa nyara pia na kuachiliwa huru tarehe 29 Oktoba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jumapili usiku, boti tatu zilizoporwa zilirudishwa ingawa mafuta yenyewe, vifaa vya mawasiliano na baadhi ya silaha hazikurudishwa.

UNMISS imetoa wito vifaa hivyo virudishiwe mara moja, huku mkuu wa UNMISS Ellen Loej akikariri kwamba pande za mzozo Sudan Kusini zinapaswa kuhakikishia uhuru wa misafara ya Umoja wa Mataifa nchini humo.