Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zanzibar yafuta uchaguzi, UM wazungumza

Zanzibar yafuta uchaguzi, UM wazungumza

Tume ya uchaguzi Zanzibar, ZEC, imefuta uchaguzi uliofanyika visiwani humo tarehe 25 mwezi huu ambapo Umoja wa Mataifa umesema unafuatilia kuweza kufahamu maana ya hatua hiyo kwa kuwa wapiga kura walichagua pia Rais wa Muungano na wawakilishi wa katika bunge la Tanzania.

Akizungumza na Idhaa hii, mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Alvaro Rodriguez amesema..

(Sauti ya Alvaro)

Tume ya uchaguzi Zanzibar imefuta matokeo ya uchaguzi kutokana na kasoro nane au tisa ambazo imesema ni msingi wa kufuta. Lakini hatufahamu athari zake kwa kuwa walikuwa wanachagua nafasi kadhaa kwa kuzingatia mfumo wa Muungano wa Tanzania. Hatuna uhakika iwapo chaguzi zote tano katika Pemba na Unguja zimefutwa au kura tu ya Rais wa Zanzibar ambayo imekuwa na ushindani na kutangazwa sana na vyombo vya habari.”

Kasoro zilizotajwa ni pamoja na baadhi ya vituo kukiuka kanuni na mmoja wa wagombea urais kujitangaza mshindi kwa hiyo Bwana Alvaro amesema kile wanachofanya sasa.

(Sauti ya Alvaro)

Lengo letu sasa ni kuzungumza na wadau mbali mbali kufahamu hali ilivyo na aina ya ushauri tunaoweza kuwapatia wadau wetu mbali mbali ili kuweza kuendelea  kusaidia maendeleo ya amani na demokrasia nchini Tanzania.”

Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, ZEC inasimamia  uchaguzi wa rais wa Zanzibar, madiwani na wawakilishi, ilhali Tume ya Taifa ya uchaguzi, NEC inasimamia uchaguzi wa Rais wa Muungano na wabunge ambapo wapiga kura wa Zanzibar hupiga kura kuchagua nafasi zote tano.