Skip to main content

Vifo kutokana na TB vimepungua kwa takriban nusu tangu 1990- WHO

Vifo kutokana na TB vimepungua kwa takriban nusu tangu 1990- WHO

Vita dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu, yaani TB, vinaonekana kupata ufanisi mkubwa, kiwango cha vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kikiwa kimepungua kwa kiasi kikubwa hadi takriban nusu ya idadi ya vifo vya mwaka 1990.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2015 ya Shirika la Afya Duniani, WHO kuhusu TB duniani, ambayo imetolewa mjini Washington, DC, Marekani, ikionyesha pia kuwa vingi vya vifo hivyo vingaliweza kuzuilika.

Aidha ripoti hiyo ya kila mwaka imesema ili kupunguza mzingo wa TB kwa ujumla, mapengo ya upimaji na matibabu yanapaswa kuzibwa, huku ufadhili ukijazwa, pamoja na kubuni upimaji, dawa na chanjo mpya.

Ripoti imeongeza kuwa mafanikio makubwa yamekuja tangu mwaka 2000, ambapo malengo ya maendeleo ya milenia yalipopitishwa.

Kwa ujumla, maisha ya watu milioni 43 yaliokolewa kati ya 2000 na 2015 kwa upimaji na matibabu yapasayo.