Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vurugu haikuwa nyingi wakati wa uchaguzi Haiti: MINUSTAH

Vurugu haikuwa nyingi wakati wa uchaguzi Haiti: MINUSTAH

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti MINUSTAH umesema leo kwamba uchaguzi wa jumapili tarehe 25, Oktoba nchini humo umefanyika bila machafuko makubwa.

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, vituo vyote vimefungua na kufunga katika muda uliotakiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini New York, bwana Dujarric ameongeza kwamba, ingawa kiwango cha ushirikiano katika uchaguzi hakijatangazwa, wafuatiliaji wengi wameona kwamba watu wengi zaidi wamekuja kupiga kura kuliko uchaguzi wa tarehe 9 Agosti ambapo asilimia 18 tu ya watu wamepiga kura.

Kwa ujumla, polisi 10,000 kutoka kwa serikali na MINUSTAH wameshiriki ili kuhakikisha usalama wa uchaguzi.

Hata hivyo, vitendo 48 vya uvunjaji usalama vimeripotiwa, vikiwa vimepungua kwa nusu tangu uchaguzi uliopita.

Awamu ya pili ya uchaguzi wa rais utafanyika tarehe 27 Disemba ikihitajika.