Mlipuko wa Polio Somalia watokomezwa:UM

Mlipuko wa Polio Somalia watokomezwa:UM

Wataalamu wa afya wametangaza kuwa Somalia imetokomeza rasmi mlipuko wa Polio ulioripotiwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2014.

Tangazo hilo limekuja miezi 14 tangu kutangazwa kwa mgonjwa wa mwisho kufuatia mlipuko huo uliokumba takribani watu 200.

Jopo la wataalamu kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la Afya WHO na lile la watoto UNICEF pamoja na washirika wake lilitathmini na kusema sababu ya kushinda mlipuko huo ni juhudi za pamoja kati ya serikali, wahudumu wa afya na wazazi katika kuhakikisha watoto wanapata chanjo dhidi ya Polio.

Mwakilishi wa WHO nchini Somalia Ghulam Popal ametoa pongezi kwa juhudi hizo alizosema zilifanyika licha ya changamoto ya usalama nchini humo.

Zaidi ya watoto Milioni 2 wenye umri wa chini ya miaka mitano walipatiwa chanjo katika kampeni kamambe zilizoendeshwa na mashirika hayo na wadau wake.